CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) katika Wilaya ya Moshi kimedai kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe amefilisika kisiasa na kumshauri kurejea katika biashara zake.
Akizungumza mbele ya wajumbe wa sekretarieti ya CCM ya Wilaya ya Moshi Mjini, Katibu wa CCM wilayani humo, Aluu Segamba alisema Chadema inatafuta kisingizio na kujenga chuki kwamba CCM itaiba kura mwaka 2015 jambo ambalo alisema halijawahi kufanyika.
Kauli ya CCM imetolewa siku chache baada ya Mbowe kutamka katika mikutano yake mikoa ya Kusini kwamba iwapo CCM itasalimika mwaka 2015, atajiuzulu siasa.
“Mbowe alishashindwa siasa muda mrefu kwa hiyo asitafute kisingizio... ajue tu mwaka 2015 CCM itashinda nafasi ya urais na wabunge likiwamo Jimbo la Hai analoliongoza kwa sasa… huyu fani yake ni biashara aende huko,” alisema Segamba.
Alisema jambo wanalolalamikia Chadema kwa sasa la ugumu wa maisha ni la dunia nzima na kutoa mfano kwamba bei ya sukari nchini ni Sh 2,100 wakati Kenya ni Sh 3,000.
Aliongeza kuwa hata mfumuko wa bei nchini ni asilimia 20 wakati Kenya ni asilimia 22 na kuhoji na huko nako kuna CCM? Segamba alikitaka chama hicho kueleza wananchi hoja za msingi badala ya kuwadanganya na kuwajaza chuki kwa masuala ambayo yapo wazi haswa kupaa kwa bei ya bidhaa kunakotokana na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.
“Hoja kwamba enzi za Mwalimu Julius Nyerere hakukuwa na matatizo siyo sahihi… hawakumbuki wakati wa unga wa njano, sabuni na matatizo mengine lakini hayo ni ya wakati huo, leo hii suala la mafuta ni la dunia Serikali inafanya kazi nzuri na wananchi wanaona,” alisema.
Alitoa mfano kuwa Serikali kwa sasa imewafikisha mahakamani viongozi wanaokabiliwa na tuhuma mbalimbali zikiwamo za kupoteza mapato na miongoni mwao wapo mawaziri, makatibu wakuu, wabunge na wakurugenzi wa halmashauri za wilaya.
Katika hatua nyingine, Katibu huyo alisema Chadema ambayo imeliongoza Jimbo la Moshi mjini kwa miaka 15 haijajenga hata choo au barabara ya urefu wa kilometa moja huku hali za maisha za wakazi hao zikiendelea kuwa duni.
Soma zaidi ...http://www.habarileo.co.tz