MADAKTARI
146 wamefukuzwa katika hospitali mbalimbali nchini kutokana na
kushiriki mgomo unaoendelea nchi nzima kwa lengo la kuishinikiza
Serikali kutekeleza madai yao.
Uchunguzi
wa Mwananchi umebaini kuwa, madaktari hao walitimuliwa katika Hospitali
za Bugando na Sekou Toure mkoani Mwanza na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa
wa Mbeya na ile ya Rufaa Dodoma.
Wakati
Serikali ikichukua hatua hiyo, mgomo huo jana uliendelea katika
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Ocean Road, Taasisi ya Mifupa
Muhimbili (MOI) za jijini Dar es Salaam, Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na
Hospitali ya Rufaa ya KCMC mkoani Kilimanjaro.
Katika
kile kinachoonekana kuwaunga mkono wenzao, madaktari bingwa wa MOI, MNH
na Ocean Road jijini Dar es Salaam, jana walitangaza rasmi kuingia
kwenye mgomo huo hadi madai hayo yatekelezwe.
Madai
ya madaktari ni hali bora ya mazingira ya utoaji huduma nchini,
ongezeko la mishahara, posho za kufanya kazi katika mazingira magumu,
posho za kufanya kazi katika mazingira hatarishi na posho za kuitwa
kazini.
Tamko
la madaktari hao bingwa, lilitolewa jana na msemaji wao, Dk Catherine
Mng'ong'o muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao chao kilichofanyika
jijini Dar es Salaam.
Tamko
hilo limekuja siku moja baada ya baadhi yao kuanza kushiriki mgomo huo
juzi, kushinikiza pamoja na mambo mengine, Serikali itoe tamko juu ya
tukio la kutekwa na kujeruhiwa kwa Dk Ulimboka.
Hata
hivyo, wakati madaktari hao wakitoa tamko hilo, uongozi wa Moi jana
ulitoa tangazo kuwataka madaktari wote walioshiriki mgomo huo kurejea
kazini ifikapo Julai 2, mwaka huu, vinginevyo watafukuzwa kazi.
Jana
jengo la MOI lilikuwa limefungwa kwa makufuli, huku wagonjwa wakielezwa
kuwa huduma zote hazitolewi zikiwamo za dharura ambazo awali
ziliendelea kutolewa.
Mmoja wa walinzi aliwambia waandishi wa habari kuwa, amefunga mageti kutokana na amri ya mkuu wake wa kazi.
“Mimi
ninatekeleza amri ya bosi wangu, amenitaka kufunga geti na hakuna mtu
kuingia, awe mgonjwa au ninyi waandishi wa habari kwa kuwa hakuna huduma
zinazotolewa humu,” alisema.
Mkoani Mwanza
Madaktari
63 walio katika mafunzo ya vitendo kazini wa Hospitali ya Rufaa ya
Bugando, Hospitali ya Mkoa Sekou Toure wametimuliwa na kurejeshwa
wizarani kutokana na mgomo huo.
Mkurugenzi
wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Dk Charles Majinge alisema kuwa, juzi
aliwataka madaktari waliokuwa katika mgomo kurejea kazini, lakini
hawakufanya hivyo na jana akaamua kuwarejesha 47 wizarani.
Katika
Hospitali hiyo ya Mkoa wa Mwanza Sekou Toure, Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk
Valentino Bangi alisema, madaktari 16 wamesimamishwa kufanya kazi
kutokana na agizo la wizara.
Kilimanjaro
Madaktari
walioko kwenye mgomo katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Moshi mkoani
Kilimanjaro walisema jana kuwa, kinachofanywa na Serikali kuwafukuza
kazi waliogoma, ni njia mojawapo ya vitisho, lakini wakasema kuwa kamwe
hawataogopa.
Madaktari
hao ambao hawakutaka majina yao yaandikwe gazetini walisema, wao
wanaendelea na mgomo mpaka pale Serikali itakapotekeleza madai yao.
“Tumesikia
wenzetu wa Dodoma na Mbeya wamefukuzwa ….Hiyo haitufanyi turudi kazini
na kama Serikali inaona hiyo ndiyo njia ya kumaliza mgogoro huu
waendelee sisi tutarudi kazini pale itakapotimiza tunayotaka,” alisema
mmoja wa madaktari hao.
Mbeya
Juzi
Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, ilitoa tangazo la kuwataka madaktari
waliopo mafunzoni waliogoma kurejea kazini jana, na endapo wangekiuka
agizo hilo wangekuwa wamejifukuzisha kazi. Na hadi jana jioni hospitali
hiyo ilikuwa imewafukuza madaktari 72.
Ocean Road
Katika
Taasisi ya Taifa ya Saratani, (Ocean Road), kutokana na madaktari sita
kusitisha kutoa huduma tangu Dk Ulimboka alipojeruhiwa kwa kipigo,
waligoma na jana Mkurugenzi wa Tiba na Huduma Diwani Musemo alionekana
akitembelea wagonjwa.
Dodoma
Madaktari
11 wa mafunzo kwa vitendo katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma nao
wamefukuzwa, tukio ambalo jana lilileta usumbufu mkubwa katika
upatikanaji wa tiba hospitalini hapo.
“Kwa
hakika matibabu yanaendelea ingawa ni katika hali ya kusuasua. Hatuna
uhakika kama kweli kuna mgomo wa chinichini au la, maana mimi nimefika
mapema, lakini bado sijahudumiwa," alisema mmoja wa wagonjwa
waliozungumza na mwandishi wa habari.
Arusha
Katika
Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, huduma zimedorora lakini
Mganga Mkuu, Dk Omar Chande alisema jana kuwa, imekuwa ni vigumu
kuchukua hatua kuwabana madaktari ambao wanatuhumiwa kufanya mgomo
baridi, kwani wote wanaripoti kazini.
"Ni
kweli kuna taarifa hizi za kuwapo mgomo baridi, lakini madaktari wote
wapo kazini, ila kama kuna kufanya kazi chini ya kiwango, tumeanza
uchunguzi," alisema Dk Chande.
Amana
Katika
Hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam utoaji wa huduma ulisuasua
kutokana na mgomo huo jambo lililofanya uongozi kuweka tangazo kwenye
Ofisi ya Mganga Mkuu kuwataka watumishi wote ambao hawakuwapo kazini
kuanzia Juni 25, 2012 waandike barua za kurejea kazini.
Tangazo
hilo pia linawataka madaktari walioko mafunzoni kuandike barua kwenda
kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupitia kwa mganga
mkuu wa hospitali hiyo.
Habari
hii imeandaliwa na Frederick Katulanda, Mwanza, Rehema Matowo, Moshi,
Zakhia Abdallah (SJMC), Editha Majura, Israel Mgussi, Dodoma), Victoria
Mhagama na Daniel Mwingira, Sam Jacob na Issa lazaro (SJMC, Godfrey
Kahango, Mbeya, na Mussa Juma, Arusha.