AFRIKA YAANGUKIA PUA KATIKA SOKA OLIMPIKI.
WAWAKILISHI wa Afrika waliokuwa wamebakia katika michuano ya soka ya Olimpiki inayoendelea jijini London, Uingereza timu za Misri na Senegal zimetolewa katika hatua robo fainali ya michuano hiyo.
Misri waliyaaga mashindano hayo baada ya kukubali kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Japan wakati Senegal wenyewe walifungwa na Mexico mabao 4-2. Kwa matokeo hayo Japan watakutana na Mexico katika hatua ya nusu fainali wakati timu ambayo inapewa nafasi kubwa ya kunyakuwa medali ya dhahabu kwa mara ya kwanza katika michuano hiyo timu ya Brazil watakutana na Korea Kusini baada ya kufanikiwa kuifunga Honduras katika hatua ya robo fainali. Korea Kusini walitinga katika hatua hiyo baada ya kufanikiwa kuwaondosha wenyeji Uingereza kwa changamoto ya mikwaju ya penati baada ya timu hizo kwenda sare ya bao 1-1 katika dakika 120 walizocheza. Nusu fainali ya michuano hiyo inatarajiwa kufanyika Jumanne ambapo Brazil na Korea Kusini watakutana katika Uwanja wa Old Traford uliopo jijini Manchester wakati Mexico na Japan wenyewe watacheza katika Uwanja wa Wembley jijini London.