Zamani ilikuwa ni kawaida kuona wanawake wanatoboa masikio, pua, ili kuvaa aina mbalimbali za herini na shemeri.
Siku hizi si ajabu kuona wanaume na wanawake wakijitoboa au kuchorwa alama (tattoo)
sehemu mbalimbali za miili yao kama kwenye pua, mdomo, ulimi, tumbo,
masikio, mikono, miguu, kwenye kichwa, mapaja, mgongo na hata sehemu
za siri yote haya kwa ajili ya urembo, miila au desturi zao, kutaka
kujinasibu na tabaka fulani au kutaka kuonyesha ubunifu wao (artistic expression).
Kutoboa/kuchorwa mwili kama kutafanywa na mtaalamu wa kutoboa/kuchora mwili hakuna madhara yoyote ya kiafya. Madhara
ya kutoboa/kuchorwa mwili hupatikana pale tu ambapo kitendo hiki
hufanywa na mtu ambaye si mtaalamu na mjuzi wa fani hii bila kutumia
njia salama za kiafya.
Ni mambo gani ya kuzingatia kabla ya kutoboa/kuchorwa mwili wako?
1.Unatakiwa kujua uwezekano wako wa kupata maambukizi
- Kama tayari una maambukizi au una kidonda kilichowazi, ni bora
ukaacha kutoboa/kuchorwa mwili mpaka utakapopona na kuwa na afya
njema.
Hatari ya kupata maambukizi ni kubwa kama utatobolewa/kuchorwa na mtu ambaye si mtaalamu na hana ujuzi wa kufanya kazi hii.
Hakikisha
anayekufanyia hivi awe anafahamu masuala ya kukinga wateja wake na
maambukizi ambayo ni pamoja na kusafisha vifaa vyake kila baada ya kazi,
kuvichemsha vifaa hivyo au kuhakikisha vipo salama na havina bakteria
wowote kwa kutumia kemikali za kusafishia, kuvifunika vifaa hivyo baada
ya kuvisafisha na yeye mwenyewe kuvaa gloves salama (surgical gloves) wakati wa kufanya kazi yake hiyo ili hata kama ana magonjwa ya kuambukiza asiweze kukuambukiza wewe kwani
2.Hakikisha huna maradhi yoyote sugu
- Kama una maradhi ya kisukari, ni bora ukaepuka kutoboa/kuchorwa
mwili kwani kidonda chake kinaweza kisipone haraka na hatari ya
maambukizi kwa wagonjwa wa sukari iko juu kupitia kwenye vidonda.
3.Fahamu kuhusu uwezo wako wa kupona - Unatakiwa uwe na ufahamu juu ya uwezo wa mwili wako katika kupona (healing tendencies) kidonda chochote kile.
Kuna
watu wengine wanapopata mchubuko au kukatika ngozi zao hupona kwa
ngozi ile kufanya kama baka na uvimbe unaojulikana kama keloids.
Kama wewe ni mmoja wa watu wa aina hii basi unahitaji kuepuka kufanya kitendo hiki cha kutoboa/kuchora mwili wako.
Sehemu
ambazo huchukua muda mrefu kupona baada ya kutoboa/kuchora mwili ni
pamoja na kwenye maeneo ya tumboni, kwenye chuchu na hata sehemu za
siri kwa wanawake.
4.Jua maumbile yako-Sio
kila ngozi ya mwanadamu inafaa kwenye kuitoboa/kuchora, mfano, wale
wenye ngozi ya kwenye tumbo iliyoenuka ndio hufaa kutoboa sehemu hii,
kama unataka kutoga ulimi na ulimi huo ni mfupi kutokana na umbile
lako, (Tongue with short frenum) yaani wale wenye mkunjo chini ya ndimi zao na hivyo kufanya ulimi kuwa mfupi, hawapaswi kutoga ndimi zao.
5.Hakikisha unafanyiwa na mtaalamu wa fani hii.Wataalamu
wa mambo ya kutoboa/kuchora mwili wana uelewa mkubwa wa maumbile ya
mwanadamu na huwa na vifaa vya kuzuia uvujaji wa damu pindi unapotokea.
Pia huwa na ufahamu wa jinsi ya kukulinda na maambukizi .
6.Historia yako ya afya-
Wataalamu wa kutoboa/kuchora mwili wanatakiwa kuchukua historia ya
afya ya wateja wao inayohusisha magonjwa ya moyo, ugonjwa wa kisukari,
mzio/aleji, ugonjwa wa pumu na kadhalika.
Kama
unatumia dawa za ugonjwa wowote ule ni bora ukamweleza mapema mtaalamu
huyo kabla hajaanza kukutoboa/kukuchora mwili wako.
Ili kuzuia uvujaji wa damu kwa wingi, unashauriwa kuepuka dawa aina ya aspirin angalau kwa wiki moja kabla ya kutoboa/kuchora mwili wako, pia epuka dawa jamii ya Non Steroidal Anti-Inflammataory Drugs (NSAIDS) kama ibuprofen, naproxen na kadhalika.
7.Hakikisha vifaa sahihi ndivyo vilivyotumiwa-
Hakikisha ya kwamba vifaa vinavyotumiwa ni vile ambavyo havina
madini ya Nickel, pini zenye ubora na vipachiko vya aina mbalimbali
ambavyo ni vya ubora wa hali ya juu.
Pini na vipachiko vidogo vinaweza kutoka na kusogea kutoka katika sehemu vilipopachikwa na hivyo kukuletea madhara makubwa.
8.Mfumo wa maisha-
Kipachiko cha katika maeneo ya tumboni (kitovuni, chini ya kitovu nk)
huvutia kwa mwanamke wenye umri mdogo wa miaka ya ishirini na huleta
picha mbaya kwa wanawake wale waliofikia umri wa miaka thelathini na
kuendela.
Unatakiwa
uangalie na aina ya taaluma yako kama inaendana na vitu vya aina
hivi, mathalani wewe ni mwanamume unafanya kazi ya mhudumu wa afya,
mwalimu, askari, unafanya kazi kwenye ofisi, muuzaji bidhaa kwa
wateja, mtoa huduma za kijamii, halafu unavaa herini kwenye masikio,
ha! Watu watakuchukuliaje?
Hakuna
atakaye kuelewa au kukubali kuhudumiwa na wewe. Pia angalia kama
mila, desturi, dini yako kama inakubali mambo haya kwani itakuwa
jambo la aibu sana kama utatoga mwili wako bila kuzingatia mazingira
unayoishi kwani binadamu tunaishi kulingana na mazingira yetu.
Hii
sio kwa wanaume tu hata kwa wanawake, kabla ya kutoboa/kuchora sehemu
husika zingatia taaluma yako, mila, desturi,mazingira, dini yako nk.
9.Fuata maelekezo vizuri-
Fuata maelekezo unayopewa vizuri jinsi ya kujikinga na maambukizi
baada ya kutoboa/kuchorwa mwili wako, namna ya kusafisha sehemu husika
nk.
10.Fahamu madhara ya kutoboa/kuchorwa sehemu husika-
Fahamu kuhusu madhara ya kutoboa/kuchorwa sehemu husika kwanza kabla
ya kutoboa/kuchorwa ili uweze kujiepusha na madhara hayo.
Pia
unatakiwa ujue sehemu hiyo unayotoboa/kuchora, kidonda chake kinapona
baada ya muda gani na maumivu yake huchukua siku ngapi kuisha?
Hatma ya afya yako ipo mikononi mwako! Tafakari!