BOLTON KUMPA KIBARUA MUAMBA.
KLABU ya Bolton
Wanderers inatarajia kuzungumza na Fabrice Muamba ili aweze kubaki
katika klabu hiyo yenye maskani yake katika Uwanja wa Reebok kwa
shughuli zingine baada ya kutangaza kustaafu soka. Muamba mwenye miaka
24 ambaye alikuwa akicheza nafasi ya kiungo katika klabu hiyo alitangaza
kustaafu soka jana ikiwa imepita miezi mitano toka alipoanguka na moyo
wake kushindwa kufanya kazi kwa muda wa dakika 78. Mchezaji huyo anaweza
kuwa mbali na mambo ya kucheza soka lakini anaweza kupewa kazi ya kuwa
balozi au shughuli za ukocha katika klabu hiyo. Meneja wa Bolton, Owen
Coyle amesema kuwa wamezungumza na Muamba na anajua kuwa klabu hiyo
itamsaidia kwa kitu chochote ambacho atahitaji katika kipindi hiki
kigumu ambacho kinamkabili. Klabu ya Bolton na Muamba mwenyewe
wanatarajiwa kulipwa bima ambayo inakisiwa kuwa mamilioni ya paundi za
Uingereza kutokana na sakata hilo.