Sitta:Msiisubiri Serikali Kutaja Walioficha Mabilioni


WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amewataka wanaotangaza kuwafahamu vigogo walioficha mabilioni ya fedha nje ya nchi kuwataja mara moja ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao badala ya kuisubiri Serikali kufanya hivyo.Kauli hiyo ya Sitta ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Mashariki (CCM), imekuja wakati baadhi ya wanasiasa, wakiwamo wabunge kutishia kuwataja watu hao, lakini wakisisitiza kuwa ni pale tu Serikali itakaposhindwa kufanya hivyo.
Utafiti uliofanywa na Shirika la Kimataifa la Fedha la Global Financial Integrity, unaonyesha kuwa tatizo la utoroshaji wa fedha nchini limekuwapo katika awamu zote za Serikali zilizoiongoza Tanzania, lakini Awamu hii ya Nne imetia fora.

Utafiti huo uliofanywa kuanzia mwaka 1970 hadi 2009, unaonyesha kuwa katika utawala wa Rais Jakaya Kikwete, fedha zilizofichwa nje ya nchi ni Dola za Marekani 7,967.4 milioni (sawa Sh12.7 trilioni).
Akizungumza katika mahojiano maalumu, kuhusu nini kifanyike ili kuiokoa Tanzania isiendelee kufilisiwa na watu wachache, Sitta alisema anasikitishwa na watu hao kuogopa na kuwaficha watu wanaofisadi mali za nchi na hasa pale inapokuwa wahusika ni vigogo wa Serikali.

Alisema vigogo hao ni sababu ya watu kupata kigugumizi katika hili akihoji : “Kwa nini linapokuwa ni suala linalowahusu hawa wanaoitwa vigogo hawatajwi?”

Sitta ambaye ameshika nyadhifa mbalimbali serikalini katika awamu tofauti, alisema haoni kama kuna kosa kumtaja hadharani mtu aliyeficha fedha nje ya nchi huku akisababisha Watanzania kuendelea kukabiliwa na maisha magumu.

“Watajwe! Kama ni Samuel Sitta ameficha fedha nje atajwe. Kwa kweli mimi sioni kama kuna dhambi yoyote kumtaja,” alisema Sitta huku akisisitiza kwamba huo ni msimamo wake binafsi unaotokana na uzoefu wake kwenye uongozi wa nchi na siyo kwa mamlaka aliyonayo ya Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Alisema njia nzuri ya kukomesha tabia hiyo ni kuwataja na vyombo husika kuwafikisha mahakamani kwa kuzingatia kuwa sheria ni msumeno, haipaswi kubagua aliye mdogo au mkubwa kwa maana ya wadhifa katika nchi.Sitta ambaye pia aliwahi kuwa Spika wa Bunge alisema: “Swali la kwa nini hawatajwi, ni jambo la kushangaza.”

Alisema amesikia na kuwasoma baadhi ya wanasiasa wakitishia kuwa watawataja wahusika iwapo Serikali haitafanya hivyo, lakini akasema haoni sababu yoyote ya mtu kusita katika kuokoa taifa dhidi ya wizi wa fedha za umma.

“Haiwezekani kwa mwanasiasa yeyote katika nchi maskini kama Tanzania au kiongozi wa Serikali kuwa na utajiri wa mabilioni ya fedha.”

Alisema hata kama anafanya biashara, siyo rahisi kuwa na utajiri wa kiwango hicho hasa ikizingatiwa kuwa hutumia muda mrefu kulitumikia taifa.
“Sisi tunaofanya kazi serikalini, tunatoka saa moja usiku. Sasa muda huo wa kufanya biashara ni saa ngapi?”

Tuhuma hizo ziliibuka bungeni Jumatano iliyopita baada ya Kambi ya Upinzani kudai kwamba nawafahamu wahusika wa ufisadi huo na kutishia kuwataja ikiwa Serikali haitafanya hivyo.