Nchi Tatu Zakabidhiwa Tuzo


Nchi tatu zimekabidhiwa Tunzo kutokana na ubunifu wao katika Sekta ya Umma .
Nchi hizo zilizoshinda na kupewa Tunzo na Jumuiya ya Utumishi wa Umma katika Afrika na Uongozi AAPAM ni pamoja na Kenya, Mauritius na Ghana
Tunzo hizo zimetokana na kuwa wabunifu katika masuala mbalimbali ambapo Kenya imekuwa mshindi wa Kwanza kwa kupata medali ya dhahabu ikifuatiwa na Mauritius iliyopata Medali ya Fedha na Ghana iliyopata Medali ya Shaba.

Wakati huo huo Mkutano wa 34 wa AAPAM uliomalizika hivi leo hapa Zanzibar na kufungwa rasmi na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Balozi Seif Ali Idd umetoa maazimio mbalimbali yanayohusu Mkutano huo.

Miongoni mwa maazimio hayo ni kuwa na Mfumo bora na mzuri wa Utawala, kuimarisha mazingira juu ya nchi na Uongozi, Kuwashirikisha wadau wengine katika kuimarisha Utawala Bora na siyo Serikali kujipangia wao wenyewe tu.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa AAPAM ameeleza kuwa Mkutano huo wa 34 umefanikiwa sana kutokana na mahudhurio ambapo Wajumbe 420 walihudhuria kutoka nchi 35 za Afrika na nje ya Afrika.

Mwaka jana Mkutano kama huo wa AAPAM uliofanyika nchini Malawi nchi 35 zilihudhuria ambapo wajumbe wapatao 210 ndio walioshiriki.

Katibu huyo wa AAPAM ameeleza kuwa tangu kufanyika Mikutano hiyo hii ni mara ya kwanza kwa wajumbe wengi kuhudhuria katika Mkutano huo na kuwa wa mafanikio makubwa.

Mkutano wa AAPAM hapo mwakani umeamuliwa kufanyika mjini Kigali,Rwanda. 

Wajumbe kadhaa waliohudhuria Mkutano huo wameshaanza kuondoka hapa Zanzibar kurejea nyumbani.

IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR.