TOTTENHAM YAMTIMUA REDKNAPP.

 
MENEJA wa klabu ya Tottenham Hotspurs, Harry Redknapp ameikacha klabu hiyo baada ya kuifundisha kwa muda wa miaka mine baada ya kushindwa kufikia makubaliano katika mkataba wake mpya. Redknapp mwenye umri wa miaka 65 ambaye aliwahi pia kuinoa klabu ya West Ham alifanya
mazungumzo na mwenyekiti wa klabu hiyo Daniel Levy ili kujua hatma ya mkataba wake ambao ulikuwa umebakiza miezi 12, huku akiamini kuwa alikuwa amefanya kazi nzuri kuinoa klabu hiyo msimu uliopita. Lakini inasemekana kuwa Levy hakufurahishwa na suala la Redknapp kushindwa kuiwezesha timu kupata nafasi ya kushiriki michuano ya Klabu Bingwa Ulaya na kukaa kwenye nafasi ya tatu kwa muda mrefu kwenye msimamo wa Ligi Kuu nchini Uingereza msimu uliopita. Spurs walimaliza nafasi ya nne katika msimamo wa ligi hiyo, kwa maana waliweza kupata nafasi ya kushiriki ligi ya mabingwa lakini wakaikosa nafasi hiyo baada ya Chelsea waliokuwa nyuma yao kubeba ubingwa wa ulaya jijini Munich dhidi Bayern. Mpaka sasa Redknapp bado anafanya mazungumzo ya juu ya malipo yake atakayoyapata baada ya Spurs kumtimua kibarua, ambapo taarifa rasmi za kutimuliwa zitatangazwa baadae leo. Meneja wa klabu ya Everton, ndio anatajwa kuwa ndio kocha anayeweza kurithi mikoba ya Redknapp katika klabu hiyo.