WILSHERE APEWA ONYO NA UEFA.


NYOTA wa klabu ya Arsenal, Jack Wilshere ameadhibiwa kutokana na utovu wa nidhamu na Shirikisho la Soka barani Ulaya-UEFA baada ya kuvunja sheria kwa kutabiri mchezo wa timu yake katika mtandao wa kijamii wa Twitter.
Maofisa wa UEFA walimuandikia barua ya onyo kiungo huyo wa kimataifa wa Uingereza mwenye miaka 20 kwa kumtabiria mchezaji mwenzake wa Arsenal wakati wa mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita. Wilshere ambaye alikosa michuano ya Ulaya mwaka huu kutokana na kuuguza majeraha ya kifundo cha mguu alipewa onyo hilo kwa kuwafanya maofisa hao kuhisi kwamba mchezo huo unaweza kuwa ulipangwa. Kiungo huyo alituma ujumbe kwenye twitter akidai kuwa anaweka kiasi cha paundi 10 akitabiri mchezaji mwenzake wa timu hiyo Emmanuel Frimpong angeshinda bao la kuongoza wakati mchezo dhidi ya klabu ya Olympiacos ya Ugiriki uliochezwa Desemba 6 mwaka jana. Sheria za UEFA zinambana mchezaji yoyote kutabiri mchezo wa timu yake kabla ya mchezo hata kama mchezaji mwenyewe hachezi kwenye mchezo huo. Kwasasa Wilshere amefunga akaunti yake katika twitter toka mwezi uliopita kutokana na sababu ambazo haziko wazi.