Miss Popular, Diamond na Raqey wakifuatilia usaili kwa makini
Msanii Nasib Abdul ambaye anajulikana zaidi kisanii kama Diamond
Platnumz Juzi Jumamosi alifanikisha usaili wa vijana mbali mbali wa
kiume na kike katika kusaka vipaji ambavyo vitashiriki katika video yake
mpya inayotarajiwa kufanyika wiki kadhaa kuanzia mwezi ujao.Usaili huo maalum ambao ulifanyika katika mgahawa maarufu wa chakula wa Nyumbani Lounge ulianza majira ya saa tano na nusu ambapo vijana wengi wa kike na kiume walijitokeza kujaribu nafasi yao ili kuwa moja kati ya watakaopewa mkataba rasmi kwa ajili ya video ya wimbo ambao Diamond na menejimenti yake hawajataka kuuweka wazi.
Katika usaili huo kulikuwa na majaji watano ambao ni pamoja na Raqey Mohammed ambaye yeye ni muongozaji mkuu wa shughuli hiyo ya usaili kupitia kampuni yake ya I- View Media ambayo ndio inajukumu la kurekodi video hiyo ya Diamond akifuatiwa na mbunifu mahiri wa mavazi Ally Remtulla. Wengine ni mkufunzi wa dance mchezaji wa Breakdance wa kitambo Sammy cool, Diamond mwenyewe namwana blog Miss Popular.
Zaidi ya Vijana mia walijitokeza katika usaili huo na kujaribu bahati kwa kuonyesha uwezo wao wa kucheza, ubunifu wa kuigiza pamoja na ku modo. Katika usaili huo hadi mwisho wa usaili huo jumla ya wavulana 19 na wasichana 15 walichaguliwa kwenda kwenye hatua ya mchujo wa mwisho .
Akizungumza na Mpekuzi baada ya shughuli hiyo Diamond alisema kwa ufupi tu kwamba ameamua kufanya hivyo ili kwanza kuwa mfano kwa wasanii wenyewe kwa kufanya kazi ki ‘profesheno’ zaidi, lakini pili ameamua kutengeneza ajira kwa vijana ambao yeye mwenyewe amekuwa akiwatumia katika shoo zake na kuamua badala ya kwenda sehemu na kurekodi video ni bora afanye nao kazi rasmi katika mazingira ya kiutaalamu na pia kwa malipo ambayo yatakuwa ndani ya mkataba.
Diamond pia aliongeza kuwa video hiyo itakuwa na hatua kadhaa ambazo ni pamoja na usaili, kujiweka sawa maana ya kujitaarisha kimwili kwa ajili ya video akimaanisha kupiga gym zaidi, kutafuta pamba kali zitakazo mg’arisha yeye pamoja na washiriki watakaobahatika kuwa katika Video hiyo ya wimbo wake pamoja na kusafiri kurekodi katika nchi tofauti ikiwemo Tanzania, bara la Afrika pamoja na Ulaya.
Mpekuzi pia ilipata nafasi ya kuongea na Raqey Mohammed, mkurugenzi mkuu wa kampuni ya I- View Media ambao ndio wasimamizi wakuu wa shughuli hiyo ambapo alisema yeye kama mtayarishaji mkuu amejipanga vya kutosha kufanya video hiyo katika next level ambapo ameshachagua location, script ipo tayari na kwa mara ya kwanza atatumia vifaa vipya kabisa vya hali ya juu katika kuandaa video hiyo.
Pia amesema ataacha jukumu la kurekebisha ama kuedit rangi ifanywe na kampuni yenye utaalamu wa hali juu katika masuala hayo katika nchi za ng’ambo.
Raqey pia aligusia kwa kusema video hiyo itachukua msichana mmoja tu na wavulana kumi na pia itatumia siku tatu kufanyika nchini Tanzania na siku nyingine itakwenda kufanyika katika nchi ambazo atazitaja baadae na kwamba zoezi zima kwa upande wake litakuwa ni la wiki tatu kabla ya kuwaachia jamaa wa nje ya nchi kufanya kazi yao.