Tangu mwaka 2001 hadi sasa, LHRC
tumekuwa tukifuatilia matukio mbalimbali ya kuuawa kwa raia yanayofanywa
na vyombo vya ulinzi na usalama.
Hivi karibuni, mnamo tarehe 2 Septemba, 2012 tulishuhudia mauaji ya
kinyama kule Iringa yaliyofanywa na polisi kwa kutumia kile
tunachosadiki kuwa ni ‘bomu la machozi’ kwa kumuua mwandishi wa habari
ndugu Daudi Mwangosi.
Leo hii, Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu kimetoa taarifa baada ya uchunguzi na kufuatilia mwenendo wa
matukio mbalimbali ya ukiukwaji wa haki za binadamu, hususan ukiukwaji
wa haki ya kuishi (waathirika wakiwa mikononi mwa vyombo vya dola).
Taarifa rasmi imeambatanishwa.
Kwa mfano kwa mwaka huu tu hadi mwishoni mwa mwezi wa tisa takwimu za
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu zinaonyesha kuwa tayari watu 24
walikwisha uawa na watendaji wa vyombo vya ulinzi na usalama. Baadhi ya
sababu ni kushindwa kuhimili siasa za vyama vingi na ukosekanaji wa
uvumilivu wa kisiasa.
Pia, kushindwa kuwa na mipango
shirikishi ya kiusalama katika maeneo ya uwekezaji hususan kwenye
migodi na kwenye hifadhi za taifa.
Baada ya kutafakari na kuangalia uwajibikaji wa viongozi wa nchi hii,
Kituo kimechukua hatua zifuatazo, baina ya nyingine:
·
Kupeleka malalamiko kwa Mjumbe Maalum
wa Umoja wa Mataifa kwenye masuala ya mauaji ya raia yanayofanywa na
vyombo vya dola (UN-Special Rapporteur on etra-judicial killings).
Kumtaka mjumbe huyu kufanya uchunguzi na kuchukua hatua stahiki kwa
serikali ya Tanzania. Taarifa ilipelekwa tarehe 28 Septemba 2012. Na
tayari ameshaanza kupitia malalamiko ya Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu;
·
Kupeleka malalamiko kwa Mwendesha
Mashitaka wa Mahakama ya Kimataifa (ICC Prosecutor) na kumtaka kufanya
uchunguzi na kuona hatua anazoweza kuchukua, Tarehe 28 September 2012;
· Kupeleka suala hili kwenye Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu
na Haki za Watu katika kikao chake cha mwezi wa Oktoba 2012, kule Ivory
Coast na kuitaka Tume kuchunguza na kuchukua hatua ikiwemo kulipeleka
suala hili Mahakama ya Afrika;
·
Taarifa hii pia imepelekwa kwa wadau
wengine mbalimbali wa haki za binadamu kama Shirika la Kimataifa la Haki
za Binadamu (FIDH) na Ofisi za umoja wa mataifa Tanzania kwa hatua
mbalimbali.
Nchi hii inaheshimu utawala wa sheria
na katiba. Katika haki zilizoainishwa kwenye katiba ibara ya 18 ni haki
ya kutoa maoni na uhuru wa mtu kushirikiana na wengine ibara ya 20.
Matumizi ya mikutano ya hadhara na maandamano yenye kufuata taratibu za
kisheria ni njia mojawapo ya demokrasia.
Hivyo ipo haja kwa serikali kutoa
taarifa na habari kwa umma kuhusu juhudi zinazochukuliwa na serikali
katika kuwalinda wao na mali zao, kuwaletea maendeleo na kupunguza ugumu
wa maisha.