Rais Kikwete akutana na Askofu Mkuu Protase Rugambwa ikulu

 Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akimkaribisha Ikulu  Askofu Mkuu Protase Rugambwa 
 Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete katika mazungumzo na  Askofu Mkuu Protase Rugambwa Ikulu
 Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akipata picha ya kumbukumbu na  Askofu Mkuu Protase Rugambwa 
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiagana na  Askofu 
Mkuu Protase Rugambwa baada ya mazungumzo yao.

Askofu wa Jimbo la Kigoma la Kanisa Katoliki, Baba Askofu Protase Rugambwa amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kwa sera nzuri ambazo zimeuwezesha Mkoa wa Kigoma kupata miundombinu nyingi na muhimu katika kipindi kifupi.
 
Aidha, Askofu Rugambwa amesema kuwa hana shaka kuwa kwa mipango iliyopo ya Serikali ni dhahiri kuwa Mkoa wa Kigoma utakuwa unapaa kwa maendeleo hasa baada ya kuanza kufanya kazi kwa eneo la uzalishaji wa kiuchumi kwa ajili ya kuuza nje la EPZ.
 
Askofu Rugambwa ameyasema hayo leo, Alhamisi, Julai 26, 2012 wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Kikwete katika mkutano uliofanyika Ikulu, Dar es Salaam.
 
“Sina shaka kuwa kuanzishwa kwa EPZ kutabadilisha kabisa kasi ya maendeleo ya Mkoa wa kigoma na hali ya wananchi wa Mkoa huo,” amesema Baba Askofu Rugambwa ambaye pia amemshukuru Rais Kikwete kwa salamu zake za pongezi kufuatia uteuzi wa kushika nafasi kubwa zaidi ya uongozi wa Kanisa Katoliki kwenye makao ya Kanisa hilo mjini Vatican.
 
Mwezi uliopita, Kiongozi wa Kanisa katoliki, Baba Mtakatifu Papa Benedict wa XV1 amemteua Askofu Rugambwa kuwa Katibu Mwambata (Adjunct) wa Kongregasio ya Uenezaji wa Injili kwa Ajili ya Mataifa na Rais wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari, Roma. 
 
Aidha, kufuatia uteuzi huo, Papa Benedict wa XV1 amempandisha daraja Askofu Rugambwa na kumfanya Askofu Mkuu. Baba Askofu Rugambwa anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Askofu Mkuu Pierqiuseppe Vacchelli ambaye Baba Mtakatifu amekubali kujiuzulu kwake nafasi hiyo baada ya kufikisha umri wa kustaafu.
 
Askofu Rugambwa amemwambia Rais Kikwete kuwa atapanga kuondoka nchini mwezi ujao Agosti 27 kwenda Vatican tayari kuanza kazi yake mpya.
 
Rais Kikwete kwa mara nyingine amempogeza Askofu Rugambwa kwa uteuzi wake akimwambia kuwa kitendo na uamuzi wa Baba Mtakatifu umeiongezea Tanzania heshima. “Uteuzi huu ni heshima kwako na kwa nchi yetu.”
 
Rais Kikwete amemwambia Askofu Rugambwa kuwa ni furaha kwa Tanzania kwa kadri wananchi wake wanavyozidi kupata nafasi za utumishi wa kimataifa.
 
Kuhusu mipango ya maendeleo ya Kigoma, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali yake ingependa kuufanya mkoa huo, kama ilivyo mingine, mambo makubwa zaidi lakini bajeti ya serikali haitoshelezi kufanya kila kitu kwa wakati mmoja.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
24 Julai, 2012