SHIRIKISHO
la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), limetangaza maandamano ya
amani yatakayofanyika Dar es Salaam wiki hii ili kupeleka malalamiko
yake kwa Serikali ya kutokubaliana na sheria mpya ya mafao ya Mamlaka
ya Udhibiti na Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi za Jamii (SSRA).
Sheria
inayolalamikiwa na wafanyakazi inazuia wanachama wa mifuko hiyo
kujitoa uanachama na kuchukua mafao yao mpaka wafikishe umri wa
kustaafu kwa hiari wa kati ya miaka 55 na 59 na kwa lazima miaka 60 au
wanapopata ulemavu wa kudumu.
Mratibu
wa Kamati ya Tucta ya Mkoa wa Dar es Salaam, Musa Mwakalinga jana
alisema maandamano hayo yatafanyika Agosti 4 na yataanza saa 1.30
asubuhi katika ofisi za Tucta makao makuu Mnazi Mmoja hadi ofisi za
SSRA eneo la Makochi, Kinondoni barabara ya Ali Hassan Mwinyi.
Mwakalinga
alisema maandamano hayo yatashirikisha wafanyakazi, wafanyabiashara na
wakulima na kueleza kuwa wameshatoa taarifa Polisi kupata ulinzi ili
kufikisha kilio chao, kwa kuwa mabadiliko hayo yataongeza umasikini kwa
wafanyakazi pindi watakapoachishwa au kuacha kazi.
“Sisi
tunachofanya ni maandamano ya amani, hivyo hatuna haja ya kuomba
kibali, ila tulichofanya ni kuwapa taarifa tu ili watupe ulinzi,”
alisema Mwakalinga.
Katibu
Mkuu wa Tucta, Nicholaus Mgaya alisema wanabariki maandamano hayo na
wanataka mabadiliko ya haraka yafanyike kwenye sheria hiyo ya hifadhi
ya jamii, ili fao la kujitoa lirejeshwe.
Alisema
wadau na Tucta hawakuona kifungu hicho cha sheria kwa kuwa
hakikujitokeza kwa uwazi kwenye muswada au kama ilivyoelezwa na SSRA,
baada ya sheria kupita na kifungu pekee cha muswada kilichotaja suala
la mafao ya kujitoa ni cha 107 kilichotoa mapendekezo ya kufuta fao la
kujitoa kwa mfuko wa PPF.
Hivyo
alisema wadau na vyama vya wafanyakazi walielewa kuwa kifungu hicho
kinalenga kufuta fao la kujitoa kwa mfuko wa PPF tu, ambao ndio pekee
uliokuwa na fao hilo na kwamba malipo ya kujitoa yangeendelea kutolewa
kama ilivyokuwa ikifanyika kwa mifuko mingine.
Kutokana
na hilo, alisema Tucta inataka uandaliwe utaratibu mwafaka
utakaohakikisha mwanachama anayeshindwa kuendelea na uanachama wa Mfuko
anarejeshewa michango yake na ya mwajiri pamoja na riba mara tu
anapokoma uanachama wa mifuko hiyo.
Alisema
Tucta haitasita kuchukua hatua za kisheria, endapo mamlaka itaendelea
kushikilia msimamo wake wa kubakiza kifungu hicho kinachomtaka
mwanachama wa mfuko afikishe miaka 55 ndipo alipwe mafao.
Aidha,
alisikitishwa na kushangazwa kuwahishwa kutangazwa kwa mabadiliko ya
sheria ya hifadhi ya jamii, huku mchakato wake ukiwa haujakamilika
baada ya kuridhiwa na Rais, kama vile kupita kwa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali, akisema huo ni
ukiukwaji mkubwa wa taratibu.
“Hali
hii inatupa shaka kuwa huenda sheria hiyo ikawa na mabadiliko ambayo
wadau hatukuyaridhia, jambo ambalo Tucta kamwe hatutalikubali,”
alisema. Alisema Tucta inataka SSRA kuchukua jukumu la kutoa elimu kwa
wanachama kuhusu sheria hiyo mpya ili kupunguza malalamiko yasiyo ya
lazima.