Maelezo Ya Mnyika Juu Ya Muswada Wa Dharura Aliouwasilisha Bungeni


TAARIFA KWA UMMA
Tarehe 03 Agosti 2012 kwa mujibu wa Kanuni ya 68 (7) ya Kanuni za Kudumu za Bunge na kwa kuzingatia kuwa marekebisho yamefanyika kwenye ratiba ya bunge ambapo Mkutano wa Bunge sasa umepangwa kuahirishwa tarehe 16 Agosti 2012 na hoja za wabunge zimeondolewa kwenye ratiba.
Nimeomba muongozo ama Serikali itoe kauli bungeni ya kutengua tangazo lililotolewa na Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) ili kuwezesha mafao ya kujitoa kuendelea kutolewa au uongozi wa Bunge uruhusu niwasilishe muswada binafsi wa sheria kwa hati ya dharura tarehe 16 Agosti 2012 kwa ajili ya kufanya marekebisho kwenye sheria husika ili kuruhusu mafao ya kujitoa kuendelea kutolewa.
Pamoja na hatua hiyo ya kuomba muongozo nimechukua hatua ya ziada ya kumwandikia Katibu wa Bunge kumweleza kusudio la kuwasilisha Muswada Binafsi wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Sheria za Hifadhi ya Jamii (The Social Security Laws (Ammendments) Act wa mwaka 2012 kwa hati ya dharura kwa mujibu wa Kanuni ya 81 ya Kanuni za Kudumu za Bunge (Toleo la Mwaka 2007).
Lengo la Muswada huo ni kufanya marekebisho yenye kuwezesha kurejeshwa kwa fao la kujitoa (withdrawal benefits) ili kuruhusu kuendelea kutolewa kwa mafao kwa mwanachama wa mfuko ya hifadhi ya jamii anapoacha kazi na kuhitaji kupewa mafao yake kabla ya kufikisha umri wa kustaafu kwa hiari (miaka 55) au kwa lazima (miaka 60) au pale anapopata ulemavu wa kudumu.
Nimeomba kupatiwa ushauri na usaidizi wa kisheria kwa mujibu wa Kanuni ya 21 (1) (d), (e) na (2) ili kuweza kuandaa Muswada Binafsi wa Sheria kwa mujibu wa Kanuni ya 81 (1), Taarifa ya Muswada huo kwa mujibu wa Kanuni ya 81 (2), hati ya kuwasilisha muswada kwa dharura na hoja ya kutengua masharti kuhusu muda wa utangazaji wa Miswada ya Sheria kwa mujibu wa Kanuni ya 81 (5) ya Kanuni za Kudumu za Bunge (Toleo la Mwaka 2007).
Kwa mujibu wa Kanuni ya 81 (5) masharti kuhusu muda wa utangazaji wa Miswada ya Sheria yanaweza kuwekwa kando na kutenguliwa kwa hoja kutolewa na kuamuliwa kama kutawasilishwa Bungeni hati iliyowekwa saini na theluthi mbili ya Wajumbe wote wa Kamati kama ni Muswada wa Kamati na kwa Muswada wa Mbunge hati iliyowekwa saini na Wabunge wasiopungua kumi inayoeleza kuwa muswada binafsi uliotajwa katika hati hiyo ni wa dharura.
Naomba kutoa taarifa kwamba kuanzia jumatatu tarehe 6 Agosti 2012 nitaanza kukusanya saini za wabunge wanaounga mkono kuwasilishwa kwa muswada tajwa kwa hati ya dharura kufanya haraka marekebisho yenye kuwezesha kurejeshwa kwa fao la kujitoa (withdrawal benefits) ili kuruhusu kuendelea kutolewa kwa mafao kwa mwanachama wa mfuko ya hifadhi ya jamii.
Nimeomba pia kwa Katibu wa Bunge kwa mujibu kifungu cha 10 cha Sheria ya ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge Cap 296 R.E 2002 kupatiwa nakala ya taarifa na nyaraka zifuatazo kwa ajili ya kujiandaa kuwasilisha muswada husika: Social Security Ammendment Act no.5 ya mwaka 2012, Sheria za Hifadhi ya Jamii zinazohusika, Taarifa na mapendekezo yaliyowasilishwa na kupelekea kufutwa kwa mafao ya kujitoa (withdrawal benefits) na maelezo kuhusu hatua ambayo kifungu husika kiliingizwa na hatimaye kupitishwa na Bunge tarehe 13 Aprili 2012.
Pamoja na kuomba taarifa na nyaraka kupitia kwa Katibu wa Bunge natoa mwito kwa wadau wa mifuko ya hifadhi ya jamii kutunipatia maoni na mapendekezo kwa ya kuzingatiwa kwenye Muswada Binafsi wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Sheria za Hifadhi ya Jamii (The Social Security Laws (Ammendments) Act wa mwaka 2012 katika kipindi cha wiki moja.
Ikumbukwe kwamba kifungu cha kufuta mafao ya kujitoa kilichozua mgogoro hakikuwepo wakati muswada uliposomwa kwa mara ya kwanza bungeni tarehe 1 Februari 2012 bali kiliwasilishwa kupitia jedwali la marekebisho ya Wizara lililowasilishwa tarehe 13 Aprili 2012 bila malengo na madhumuni yake kuelezwa kwa ukamilifu.
Kupitishwa kwa kifungu hicho kumethibitisha maneno niliyoyatoa bungeni kuwa tumefika hapa tulipo kutokana na ‘uzembe wa bunge na wabunge’ na kwa hili pamoja na mchango nilioutoa bungeni kwa maandishi siku hiyo juu ya haja ya kuwa mfumo mpana zaidi wa pensheni na hifadhi ya jamii (universal pension and social security) pamoja na kuwa sikuunga mkono kifungu husika kilichoingizwa kinyemela naomba radhi kwa wananchi wa Ubungo na wafanyakazi kwa kutokuwasilisha jedwali la marekebisho kupinga kifungu hicho kuingizwa.
Izingatiwe kuwa ili kurekebisha hali hiyo tarehe 27 Julai 2012 kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani niliitaka Serikali itoe maelezo maelezo kuhusu taarifa zilizotolewa bungeni tarehe 13 Aprili 2012 kuwa wafanyakazi ikiwemo wa migodini kupitia vyama vyao walihusishwa kutoa maoni yaliyopelekea kufutwa kwa fao la kujitoa (withdrawal benefits); suala ambalo Chama Cha Wafanyakazi wa Migodini (TAMICO) kililikanusha.
Hata hivyo, Waziri wa Nishati na Madini wakati wa majumuisho ya Hotuba yake tarehe 28 Julai 2012 hakutoa majibu yoyote bungeni kuhusu suala hilo hali ambayo imesababisha migongano kuendelea katika migodi mbalimbali kuhusu madai hayo hali ambayo kwa taarifa nilizozipata tarehe 1 na 2 Agosti 2012 inaweza kusababisha migomo migodini. Kufutwa kwa fao la kujitoa kumelalamikiwa pia na wafanyakazi na wadau wa hifadhi ya jamii katika Jimbo la Ubungo na katika taifa kwa ujumla.
Hata hivyo, suala hili na tukio husika litumike kama rejea ya bunge na wabunge kuikatalia Serikali kuwasilisha marekebisho yenye athari kubwa kipindi cha mwisho na hivyo wabunge kukosa fursa ya kupata maoni ya wananchi na pia Serikali itakiwe kuomba radhi kufuatia kulipotosha bunge kuwa wadau wa hifadhi ya jamii hususan wafanyakazi na vyama vyao walishirikishwa na kuridhia wakati ambapo wamejitokeza na kukanusha madai hayo yaliyotolewa na Wizara bungeni.
Kwa upande mwingine kufutwa kwa mafao ya kujitoa msingi wake haupo kwenye marekebisho ya sheria yaliyofanyika tarehe 13 Aprili 2012 pekee bali ni udhaifu katika mfumo mzima wa kisera na kisheria wa hifadhi ya jamii nchini hali ambayo inahitaji wadau kutaka mabadiliko makubwa.
Hivyo, naungana na wote wenye kutaka Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) kutengua taarifa kwa umma iliyotolewa ya kueleza kuwa “kufuatia kuanza kutumika kwa Sheria hiyo (ya 13 Aprili 2012) maombi mapya ya kujitoa yamesitishwa kwa kipindi cha miezi sita hadi pale miongozo itakapotolewa ili kuwezesha Mamlaka na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kutoa elimu kwa Wadau”.
Aidha, pamoja na Mamlaka kueleza kwamba sitisho la fao la kujitoa si kwa sababu za Kiserikali au Mifuko kufilisika ni vizuri mamlaka ikaeleza kwa uwazi na ukweli sababu zingine za kufanyika kwa marekebisho hayo zaidi ya ile ya kutimiza malengo ya Hifadhi ya Jamii ambayo ni kuhakikisha kuwa Mwanachama anapostaafu anapata mafao bora yatakayomwezesha kumudu hali ya maisha ya uzeeni. Tahadhari za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika taarifa za Hesabu za mwaka 2010/2011 na miaka mingine zinaashiria masuala ya ziada ambayo yanaweza kuwa yameisukuma Serikali kuja na mbinu zingine za kuhakikisha uendelevu wa mifuko ikiwemo kupitia marekebisho ya sheria za hifadhi ya jamii.
Ili bunge liweze kutimiza wajibu wa kuishauri na kuisimamia serikali kufanya marekebisho yanayostahili ya sheria husika kwa haraka ni muhimu ratiba ya bunge ikabadilishwa.
Tafsiri ya marekebisho ya ratiba yaliyofanyika ni kuwa hoja binafsi niliyoiwasilisha kwa katibu wa Bunge kutaka bunge lijadili na kupitisha maazimio ya hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa majisafi na ushughulikiaji wa majitaka haitapata nafasi ya kujadiliwa bungeni. Aidha ratiba hiyo mpya hoja binafsi iliyoelezwa kuwa itawasilishwa na Mbunge wa Kisarawe Seleman Jafo kuhusu kufutwa kwa mafao ya kujitoa kufuatia marekebisho ya sheria za Hifadhi za Jamii nayo haitawasilishwa kwenye mkutano huu wa Bunge unaoendelea kama ratiba haitafanyiwa marekebisho.
Hata hivyo, izingatiwe kuwa chanzo cha kufutwa kwa mafao ya kujitoa ni marekebisho ya sheria za hifadhi ya jamii hivyo ufumbuzi wa kurejesha fao la kujitoa unapaswa kuwa ni marekebisho ya sheria hatua ambayo njia ya haraka ya kuifikia ni kuwasilishwa kwa muswada wa sheria ama na serikali au kamati au mbunge badala ya hoja binafsi.
Hoja binafsi inaweza kuwezesha bunge kujadili na kupitisha maazimio ya kuitaka Serikali kuwasilisha marekebisho ya sheria au kuishauri na kuisimamia serikali na mamlaka zake katika utekelezaji wa sheria lakini sheria itaendelea kuwa palepale mpaka marekebisho yatakapofanywa kwa kuwasilishwa muswada wa sheria hatua ambayo nimeamua kuanzisha mchakato wa kuwezesha ichukuliwe.

Wenu katika kuwawakilisha wananchi,