MAANDALIZI
ya Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti 26, mwaka huu
yameingia dosari baada ya matukio kadhaa ya kukwamisha kazi hiyo
kujitokeza katika mikoa mbalimbali, ukiwamo Dar es Salaam ambako zaidi
ya makarani 800 wamegoma kula kiapo cha utii na kutunza siri.
Habari
zilizopatikana jana zimeeleza kuwa mbali na makarani hao, vipeperushi
vyenye ujumbe wa kutaka watu wagomee Sensa vimesambazwa mkoani Arusha,
huku mkoani Tanga kukiwa na tukio la Sheikh mmoja kutiwa mbaroni kwa
kusambaza vipeperushi vya aina hiyo.
Makarani
hao waligoma jana ikiwa ni siku yao ya mwisho ya mafunzo ya kazi ya
kuhesabu watu na makazi. Makarani hao kutoka vituo mbalimbali
kulikotolewa mafunzo hayo, walisema wameamua kugomea kiapo hicho
kutokana na fedha zilizotengwa kwa ajili ya malipo ya kazi hiyo
kuchakachuliwa kinyume na makubaliano.
Baadhi
ya vituo ambavyo makarani wake wamegoma ni Shule ya Sekondari
Makumbusho, Kambangwa, Shule ya Msingi Zawadi na vituo kadhaa vilivyopo
maeneo ya Buguruni na Kawe.Baadhi ya makarani hao walionekana wakiwa
katika makundi, muda ambao walipaswa kuendelea na mafunzo yao kabla ya
kula kiapo cha kushiriki Sensa kwa uaminifu na ukamilifu.Baadhi ya
makarani ambao waliomba majina yao yasitajwe gazetini, walisema imekiuka
makubaliano ya awali.
“Serikali
imesema imetenga Sh141 bilioni kwa ajili ya Sensa. Sisi tayari
tuliingia makubaliano nayo kwamba tunatakiwa kulipwa Sh35,000 kwa siku,
kwa muda wa siku saba jambo ambalo limegeuka na kuwa kinyume.”
“Ukipiga
mahesabu fedha ambazo tungetakiwa kulipwa kwa siku hizo saba ni
Sh245,000 lakini wao wamekuja hapa na kutupa Sh140, 000 tu. Hatuwezi
kuendelea na kazi mpaka tulipwe fedha zetu.”
Karani
mmoja katika Kituo cha Sekondari ya Kambangwa, alisema wameamua kugomea
kiapo baada ya kuona kuwa mpaka mafunzo yanahitimishwa jana, baadhi yao
hawajalipwa chochote.
RC Dar:Watalipwa
Akizungumzia
madai ya makarani hao, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki
alisema mpaka jana mchana makarani wote walipaswa kulipwa awamu ya pili
ya fedha zao. Alisema awamu ya kwanza ya malipo hayo ilifanywa katika
siku tano za mwanzo.“Kuna watu wamejichomeka katika zoezi hili, lakini
kama kweli karani ameteuliwa lazima atalipwa pesa zake na kama imetokea
amesahaulika basi afanye mawasiliano na mratibu wa Sensa wilaya
anayotoka ili alipwe,” alisema.
Sheikh mbaroni
Katika
hatua nyingine Sheikh Juma Koosa (52) anashikiliwa na polisi wilayani
Morogoro akituhumiwa kutumia kipaza sauti kuwatangazia wananchi
wasishiriki Sensa.
Sheikh
huyo ambaye pia ni mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Chuo Kikuu cha
Kiislamu Morogoro, alikamatwa Agosti 19 mwaka huu alipokuwa kwenye
Msikiti wa Miembeni, Mazinde mara baada ya kukaribishwa na wenyeji wake
kuzungumza.Imedaiwa kuwa Koosa alitoa kitabu chenye kueleza sababu za
kuwakataza Waislamu kutokushiriki Sensa mwaka huu.
Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz