Waziri
wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella Mukangara
akipokea tuzo kutoka kwa Katibu Mkuu wa International Youth Fellowship
Bw. Lee Hunmok jana wakati wa ufungaji wa kambi ya kimataifa ya vijana
Jijini Dar es Salaam. Tuzo hiyo ilitolewa kwa Wizara kama ishara ya
kutambua mchango wake katika kuhakikisha kuwa maendeleo ya vijana
yanastawi kikamilifu.
Na Concilia Niyibitanga
Maendeleo
ya vijana ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa letu, na ni muhimu
vijana wakatambua hilo kwa kutimiza wajibu wao kwa jamii
inayowazunguka.
Hayo
yalisemwa jana na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt.
Fenella Mukangara wakati akifunga kambi ya kimataifa ya vijana Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam iliyokaa kwa muda wa siku saba kwa lengo la
kuzungumzia mstakabari wa maendeleo ya vijana hususan kuwajengea
vijana fikra chanya kwa ajili ya kujiletea maendeleo.
Mukangara
alisema kuwa vijana wanatakiwa kuwa na moyo wa kujituma, kujitolea na
kufanya kazi kwa bidii ili kukabiliana na changamoto zinazowakabili
katika maisha yao ya ujana.
‘Fanyeni
kazi kwa bidii, kwa kujitolea, kwa kuzingatia muda na kujitegemea ili
kutimiza ndoto zenu za kujiletea maendeleo ya kiuchumi na kiafya’.
Alisema Dkt. Mukangara
Aidha,
amewaasa vijana kuachana na fikra za kulalamika, kudai haki bila
wajibu na kunyosheana vidole na badala yake kijana mwenyewe ajiulize
amefanya nini kutatua kero inayomzunguka.
Vijana
kataeni vitendo vya uchochezi, chuki na kejeri kwa viongozi kwani
kufanya hivyo kunaweza kuwaingiza katika misuguano isiyo na tija na
mkumbuke kuwa maendeleo ya vijana hayawezi kushamiri na kustawi pasipo
na amani, lindeni amani kwa nguvu zenu zote na kusimamia sheria wakati
wote’ Alisema Dkt. Mukangara.
Alisema
kuwa Serikali inatambua umuhimu wa vijana na kupitia Wizara yake
imeweka mipango ambayo inatoa vipaumbele kwa maendeleo ya vijana.
Naye
Katibu Mkuu wa International Youth Fellowship (IYF), Bw.Lee Hunmok
aliwataka vijana kuwatumikia wenzao na kuwa mabalozi kwa vijana ambao
hawakupata fursa ya kuingia kambini.
Bw.
Vitus Faustin Mzale ni kijana aliyeshiriki kambi hiyo kutoka mkoani
Kagera alisema kuwa ameweza kujifunza mambo mbalimbali kambini hapo na
amewataka waandaaji kushirikiana na Serikali ili kuwapa vijana mafunzo
ya ujasiriamali ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Kwa
upande wake Bi Mariza Vargas kijana kutoka Peru alisema kuwa
amefungua moyo wake kwa ajili ya kujitolea na ameweza kujua namna ya
kufanikisha malengo yake ya kujiletea maendeleo kama kijana.
Kambi
hiyo ya kimataifa iliyoandaliwa na International Youth Fellowship
ilishirikisha nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania, Kenya, Korea, Malawi,
Peru na China.