NEYMAR APIGA BAO KATIKA MICHEZO MIWILI TOFAUTI NDANI YA SAA 24.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Brazil na klabu ya Santos, Neymar ameisaidia klabu yake hiyo kushinda mabao 3-1 dhidi ya Figueirense ikiwa ni muda wa masaa 24 baada ya kuisaidia timu yake ya taifa kuifunga Sweden mabao 3-0 katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa. Neymar alikodi ndege binafsi ya kumtoa jijini Stockholm kwenda Florianopolis ambao ni mwendo wa masaa 14, kuwahi kuisaidia timu yake ambayo ilikuwa ikisuasua katika mbio za ubingwa nchini humo. Santos ambayo ilikosa huduma ya mchezaji huyo wakati akiwa katika michuano ya olimpiki wamesema kuwa safari ya ndege ya kukodi aliyochukua Neymar amelipa mwenyewe. Wakati akiwa katika ndege hiyo Neymar alipiga picha na kuituma katika mtandao wake wa kijamii wa twitter ikimuonyesha akiwa amelala ndani ya usafiri huo.