WATUHUMIWA WALIOUKATA MKONO WA ALBINO WASOMEWA MASHITAKA KWA MARA YA KWANZA.....


Wanaoonekana pichani ni watuhumiwa watano wakiwa katika Mahakama ya Hakimu wa Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa wanaotuhumiwa kuukata na kuunyofoa mkono wa mwanamke albino, Maria Chambanenge (39) (hayupo pichani) na kutokomea nao wakimwacha na majeruhi makubwa kichwani. Mkono huo waliufukia porini kijijini Miangalua ambapo ulipatikana katika msako uliofanywa na Polisi.


Watuhumiwa hao ni pamoja na mfanyabiashara aliyekuwa mteja wa mkono huo (shati la bluu), mumewe Maria (koti jeupe, fulana rangi ya machungwa), mganga wa jadi, “mchora ramani” na aliyeunyofua mkono huo.


Kesi hiyo imetajwa kwa watuhumiwa kusomewa mashitaka yanayowakabili kwa mara ya kwanza . Watuhumiwa hawakutakiwa kujibu lolote. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 6, mwaka huu.


Kabla ya kuahirishwa, Jaji alitoa ruhusa ya dhamana ikiwa na masharti kadhaa ikiwemo kila mshitakiwa kuwa na wadhamini watatu kutoka kijijini hapo, kila mdhamini kuwa na fedha taslimu ya dhamana (bond) ya shilingi milioni tatu, kila mdhamini kuwa mfanyakazi aliyeajiriwa na Serikali au shirika lolote la Kiserikali na masharti mengineyo.


Washitakiwa walishindwa kutimiza masharti ya dhamana na hivyo kurudishwa rumande hadi siku kesi yao itakapotajwa tena mahakamani hapo.