MWANAMKE AUAWA KWA KUKATWA MAPANGA NA KUNYOFOLEWA UTUMBO NA MUME WAKE HUKO KINONDONI

Marehemu Fatma Shaban akiwa na watoto wake enzi za uhai wake.
DUNIA ni mbaya, kwani haiwezi kuwa nzuri kama mauaji ya kinyama yataendelea kushamiri, binadamu wakichinjana utadhani hakuna dola wala Mungu.
 
Fatma Shaban, 24, mkazi wa Mpiji Mgohe, Kinondoni, Dar es Salaam, ameuawa kwa kukatwakatwa mapanga, viungo vyake kugawanywa kisha akatolewa utumbo.

Anayetuhumiwa kumfanyia unyama huo ni mumewe, Peter Ndala, 23, ambaye kabla ya migogoro, walishirikiana vizuri na kuchangia mambo mengi ya kimapenzi.

Unyama huo, ulitendeka Machi 7, mwaka huu, eneo la Kidimu ambalo ni mpaka unaoigawa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Habari zilizothibitishwa ni kuwa Fatma na Ndala, walikuwa wakiishi pamoja kama mke na mume, wakapata mtoto mmoja.

Uwazi halina uthibitisho kama wawili hao walifunga ndoa, ila limeelezwa kuwa Fatma na Ndala walitofautiana na kuanza kuishi kila mtu kivyake.

Habari kutoka kwa vyanzo vyetu zinasema kuwa siku ya tukio, Ndala alimtembelea Fatma kwenye sehemu yake ya biashara, alikokuwa anajishughulisha na kazi ya mama lishe.

“Alipofika pale alipewa chakula na huyo mzazi mwenzie kisha akala. Ilipofika saa 2 usiku, Fatma alifunga biashara yake na kuanza safari yake ya kwenda  nyumbani kwao ambako alikuwa anaishi kwa dada yake.

“Waliongozana pamoja, lakini wakati wanaelekea nyumbani mazungumzo yao hayakuwa mazuri, hivyo yule mwanaume akachukizwa na kuamua kumfanyia ukatili huo mzazi mwenzake,” kilisema chanzo chetu na kuongeza:

“Ndala alimkatakata Fatma, mikononi alimkata vipande viwili, akamchoma tumboni, akamtoa utumbo, baada ya hapo akatokomea kusikojulikana.

 “Fatma alipiga kelele, majirani walikimbia kwenda kumuokoa na wakakuta muuaji ametoweka.”

Chanzo chetu kiliongeza, Fatma kabla ya kufariki dunia, aliwaambia watu waliofika kumwokoa kwamba aliyemtenda unyama huo ni mzazi mwenzake kisha akamtambulisha kwa majina matatu ya Peter Ndala Kasheba.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, ACP Ulricha Matei alisema: “Ni kweli tukio hilo lilitokea na tunamsaka muuaji kwa kushirikiana na polisi wa Kinondoni.”

Credit: GPL