Diamond kuigiza kwenye filamu mpya ya Steps Entertainment


Mwanamuziki wa Bongo Flava, Diamond anatarajia kuigiza kama mhusika mkuu kwenye filamu itakayotayarishwa na kampuni ya Selles Business Inc na kusambazwa na Steps Entertainment Limited.

Akiongea kwa simu na Bongo5 jana, mtunzi na muongozaji wa filamu hiyo Selles Mapunda amesema, “mwishoni mwa mwaka jana nilikuwa na wazo la kufanya sinema, nilifanya kikao na Diamond pale Lions Hotel Sinza, tukaongea biashara nyingine, tukaenda kwenye show moja Mombasa na yeye lakini pia likaja wazo la kufanya naye sinema.”
Mapunda amesema ameifanyia kazi filamu hiyo kwa zaidi ya miezi saba na sasa yupo kwenye hatua ya mwisho ya kuikamilisha.
Amesema kwenye filamu hiyo ya Diamond atawashangaza watu kama ilivyokuwa kwenye filamu ya Crazy Tenant aliyoigiza msanii Peter Msechu na Wema Sepetu.
“Sinema ni tamu,tamu sana nawahakikishia kwamba mkiiona mtasema kwamba Diamond huyu sio yule wa muziki, huyu ni Diamond mwingine wa movie.”
Ameongeza kuwa mpaka sasa hajaipa jina filamu hiyo japo Diamond alikuwa na wazo la kuiita filamu hiyo ‘Nimpende Nani’ kutokana na wimbo alioufanya wenye jina hilo na kuongeza kuwa anategemea kutangaza jina la movie hiyo wiki ijayo.
Muongozaji huyo wa filamu amesema ilikuwa rahisi kugundua kipaji cha Diamond katika uigizaji kutokana uzoefu mkubwa alionao kwenye tasnia ya filamu.
“Mimi ni mwalimu, professional wa sinema,mimi ni mzalishaji wa wasanii wa sinema Tanzania. Mimi nimesoma sinema, tena nimesoma Nigeria kwa wamakonde kabisa wanaojua sinema zinavyofanywa . Kiulewa wangu na uwezo wangu,Diamond anaweza kufanya kitu ambacho mtu hata mmoja hakufikiria”
Amedokeza kuwa katika filamu hiyo Diamond ambaye ni mhusika mkuu ataigiza na muigizaji mmoja wapo kati ya Wema Sepetu ama Jokate Mwegelo.
“Ni Wema na Jokate, lakini mmoja anafanya mmoja hafanyi, sikuambii ni nani leo”
Mapunda amesema katika filamu hiyo Diamond atamlipa shilingi milioni tano.
“Sinema zangu zote huwa wasanii nawalipa kwanza kabla hawajaanza sinema, nawalipa advance na wanapomaliza nawalipa hela. Sijafanya sinema zile za kukopeshana.