VIGOGO WA CHADEMA WATIWA MBARONI...!



Waandishi Wetu
VIGOGO watatu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema); Mshauri wa chama hicho Dk Kitila Mkumbo na madiwani wawili, wametiwa mbaroni wakikabiliwa na tuhuma mbalimbali.Wakati Dk Mkumbo ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akiwa amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, akituhumiwa kutoa lugha ya matusi kwa mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi (CCM), Mwigullu Nchemba, Diwani wa Kata ya Mabogini Wilaya ya Moshi,  Albert Msando na Alex Umbella wa Kata ya Kirua Vunjo Mashariki, wamehojiwa na polisi kwa makosa ya jinai.


Dk Mkumbo amepandishwa kizimbani jana akiunganishwa katika kesi inayomkabili Ofisa wa Sera na Utafiti wa chama hicho kikuu cha upinzani, Mwita Waitara Mwikwabe (37).


Mwanasheria wa Serikali, Maria Mudulugu alidai mbele ya Hakimu Ruth Massamu kuwa, Julai 14 mwaka huu saa 10.00 jioni, mshtakiwa Dk Mkumbo alitoa lugha ya matusi dhidi ya mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi.


Mwanasheria aliiambia mahakama kuwa, Dk Mkumbo alitamka kuwa mbunge huyo ni malaya, mzinzi na ni 'the comedy' (msanii), huku akijua wazi kuwa kitendo hicho ni kinyume cha sheria.


Mwansheria Mudulugu alisema kuwa mshtakiwa alitoa lugha hiyo ya matusi kwenye mkutano wa hadhara wa Chadema uliofanyika katika viwanja vya kituo cha mabasi cha Kijiji cha Nguvumali Kata ya Ndago, Jimbo la Iramba Magharibi.


Mshtakiwa alikana shtaka hilo na yupo nje baada ya kudhaminiwa wa watu wawili. Kesi hiyo itatajwa tena Julai 30 mwaka huu.


Wakati huo huo, vijana wawili wakazi wa Kata ya Ndago, Paulo Nashakigwa (27) na Emmanuel  Shilla (24) wamepandishwa kizimbani katika mahakama hiyo wakituhumiwa kushiriki kumuua Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Yohana Mpinga (30).


Mudulugu alidai mbele ya mahakama hiyo kuwa Julai 14 mwaka huu, majira ya alasiri wakiwa katika Kijiji cha Nguvumali Kata ya Ndago wote kwa pamoja wakitumia fimbo na mawe, walimpiga Yohana na kusababisha afariki dunia.


Washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa vile mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.


Washtakiwa hao wameunganishwa na wenzao 12 ambao wamesomewa shtaka hilo la mauaji Julai 16 mwaka huu. Kesi hiyo itatajwa tena Julai 30 mwaka huu.


Madiwani watiwa mbaroni

Katika hatua nyingine, madiwani wawili wa Chadema wanahojiwa na polisi kwa makosa mbalimbali likiwamo la kushusha bendera ya CCM na kupandisha bendera ya taifa.
Diwani wa Kata ya Mabogini Wilaya ya Moshi, Albert Msando alikamatwa Jumanne wiki hii na kuhojiwa kwa saa mbili kwa tuhuma za kushusha bendera ya CCM.
Msando ambaye pia ni mwanasheria, anadaiwa kushusha bendera hiyo ya CCM iliyokuwa ikipeperushwa katika Ofisi ya Serikali ya Kijiji cha Chekereni kwa madai kuwa ofisi hiyo ni mali ya wananchi na si ya CCM.
Diwani huyo alilithibitishia gazeti hili jana kuhusu kuhojiwa na kusisitiza japokuwa CCM wanadai ofisi hiyo ni mali yao waliyoijenga chini ya mfumo wa chama kimoja, hawana mamlaka ya kuweka bendera yao.
“Tunakubali kuwa ofisi hii ilijengwa chini ya mfumo wa chama kimoja wakati huo ni CCM, lakini ilijengwa na wananchi wenyewe siyo CCM hivyo bendera inayostahili kupepea ni ya taifa,” alisema.
Hata hivyo baada ya diwani huyo kuhojiwa  aliachiwa bila masharti na kuelezwa kuwa jalada lake lingepelekwa kwa viongozi wa juu wa polisi kwa hatua zaidi.
Wakati huohuo, Diwani wa Kata ya Kirua Vunjo Mashariki, Alex Umbella na Mtendaji wa Kata hiyo, wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuharibu mazingira katika Shule ya Sekondari Kisomachi.
Viongozi hao wawili walikamatwa juzi saa 4:00 asubuhi baada ya kukata miti na uzio wa shule hiyo inayomilikiwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi ili kupisha upanuzi wa barabara kijijini hapo.
Mkurugenzi wa Elimu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi, Padri William Ruwaichi alidai kuwa ukataji huo wa miti iliyo mbali na barabara, ulifanywa bila kushirikisha uongozi wa kanisa.
“Sisi kama kanisa hatupingi maendeleo, lakini tunacholalamikia ni ukiukwaji wa taratibu kwa sababu huwezi kuingia kwenye taasisi yetu na kukata miti bila kutushirikisha. Tunalaani tukio hili,” alilalamika.
Ingawa Diwani Umbela hakuweza kupatikana kutokana na simu yake kuita bila kupokewa, Kamanda wa Polisi, Robert Boaz amethibitisha kukamatwa kwao.
Kamanda Boaz alisema diwani huyo na mtendaji huyo wa kata wanashikiliwa na jeshi hilo kwa mahojiano kuhusiana na tuhuma za kuharibu mazingira kwa kukata miti na uzio katika shule hiyo.
Chadema chatoa tuhuma nzito

Siku chache baada ya Mbunge wa Iramba Magharibi Mwigulu Nchemba kuwatuhumu wabunge wa Chaderma  kuwa wamemtumia ujumbe wa vitisho, chama hicho kimeibuka na kusema ujumbe huo umetumwa na mtoto wa kigogo wa CCM anayemiliki mtambo wa kuingilia mawasiliano ya watu kwa mbinu za kijasusi hapa nchini.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema Mabere Marando alisema jana kuwa mtoto huyo amenunua mtambo huo nchini Israel  na anautumia kuandaa ujumbe huo wa maneno na kuingilia mawasiliano ya simu za wabunge hao.


“Tulipopata malalamiko ya mbunge huyo wa Singida Magharibi wa kutumiwa ujumbe wa kutishiwa maisha na wabunge wetu, Tundu Lissu na John Mnyika, mimi kama kiongozi wa Idara ya Intelijensia ya  Chadema nilifuatilia. Niliwahoji (wabunge hao) wakakataa na nilipofuatilia nikagundua  kuwa ujumbe huo umetumwa kwa kutumia mtambo huo,”alisema Marando.


Marando ambaye alisita kutaja jina la mtoto huyo, jina la baba yake na cheo chake kwa madai kuwa si wakati mwafaka kwa sasa, alitaja majina ya kampuni mbili za nchini Israel alizodai ndizo zilizogundua mtambo huo.


“Nchini Israel kuna kampuni mbili ambazo ni (Verinty na Nice Systems), kampuni hizi zimegundua mtambo wenye uwezo wa kuingilia mawasiliano ya watu kwenye mitandao yao, iwe Intaneti au simu, unaweza kuandaa ujumbe mfupi na hata mrefu na kwa kutumia namba za mawasiliano za watu wengine, unaweza kuonyesha kuwa mtu mmoja amemtumia ujumbe mtu wa pili na ikaeleweka hivyo,” alisema.


Alisema kutokana na tukio hilo Chadema kimejipanga kukabiliana na kesi inayotarajiwa kufunguliwa dhidi ya wabunge hao.


“Tayari tunazo taarifa kuwa Serikali kupitia kwa Mwanasheria wake Mkuu imeanza kuandaa kesi dhidi ya wabunge hao, lengo likiwa kudhoofisha chama na juhudi za uwakilishi wao bungeni. Sisi kama chama na mimi kama mwanasheria mwandamizi tumejipanga kukabiliana na kesi hiyo,”alisema.


Habari hii imeandaliwa na Geofrey Nyang'oro, Gasper Andrew, Johnson Daniel Singida na Daniel Mjema, Moshi.