Silaha Zabadilishwa Kwa Gunia La Mahindi


WAKATI vitendo vya uhalifu vikizidi kuongezeka sehemu mbalimbali nchini, sasa silaha kutoka nchi jirani zinadaiwa kuingia kwa wingi na kuuzwa mitaani na baadhi yake kubadilishwa na mahindi, Mwananchi Jumapili limegundua.
Uchunguzi uliofanywa unaonyesha kuwa, kutokana na kushamiri kwa biashara hiyo ya silaha nchini, bunduki moja aina ya Short Machine Gun (SMG) sasa inauzwa kati ya Sh300,000 hadi Sh500,000, huku bunduki aina ya AK 47 ikiuzwa kwa Sh700,000 hadi Sh1 milioni.

Wakati vijiji kadhaa mkoani Tabora vilipokumbwa na uhaba wa chakula, bunduki aina ya SMG katika Kijiji cha Usinge wilayani Urambo zilibadilishwa kwa gunia moja la mahindi, huku AK 47 ilibadilishwa kwa magunia mawili ya mahindi.

Gazeti hili huko nyuma liliwahi kuripoti kuuzwa kwa bastola holela mitaani katika miji mikubwa ikiwamo Arusha, Mwanza, Moshi ambapo silaha hiyo ilikuwa ikiuzwa kati ya Sh800,000 hadi shilingi milioni moja.

Uchunguzi wa muda mrefu uliofanywa na Mwananchi Jumapili katika mikoa mbalimbali iliyopo mipakani umebaini kuwa, mtandao huo wa uingizaji silaha ni mkubwa na unawashirikisha matajiri na baadhi ya askari polisi wasiokuwa waaminifu.

Silaha hizo huingizwa nchini kupitia mkoani Kigoma, mpakani mwa Rwanda, Kenya, na Burundi kwa kutumia njia mbalimbali ikiwamo, magari, pikipiki na boti kupitia Ziwa Victoria pamoja na baiskeli ambapo bunduki hizo hufungwa kama mzigo ya kawaida.

Chanzo kimoja cha uhakika kililiambia Mwananchi Jumapili kuwa eneo la Usinge ndiyo kituo kikuu cha kupokelea silaha kutoka Burundi na Rwanda ambazo husambazwa mikoa mbalimbali nchini.

Mawakala
Mmoja wa watu ambao wamewahi kufanya biashara alisema kuwa mawakala wa silaha hizo wapo katika mikoa ya Kigoma na Tabora na kwamba ni wafanyabiashara, huku baadhi wakidaiwa kuwa watu wenye asili ya kabila la Kitutsi.

Lakini kwa Usinge alimtaja mfanyabiashara mmoja ambaye pia hukopesha fedha kwa riba (jina tunalo) ambaye inadaiwa kuwa biashara hiyo haramu anayoifanya inajulikana na mamlaka mbalimbali za juu serikalini.

Habari hizo zilieleza kuwa mfanyabiashara huyo amekuwa akinunua SMG kati ya Sh300,000 hadi Sh500,000, na kwamba huzisafirisha kwa kutumia mtandao wake hadi mikoa ya Kanda ya Ziwa na huziuza kati ya Sh800,000 hadi Sh1,000,000.

Mbali na kutumia silaha hizo kwa ujambazi pia huzitumia kufanya uwindaji wa tembo kwenye hifadhi za taifa na mapori ya akiba.

Habari hizo zinaeleza kuwa baada ya kuyapata meno hayo ya tembo na kukatwa vipande, husafirisha kwa kusaidiwa na maofisa wa maliasili na askari polisi wasiokuwa waaminifu.