Na: Kelvin Matandiko- Mwananchi.
JESHI
la Polisi kupitia kikosi cha Usalama barabarani nchini kimesema jumla
ya ajali za pikipiki (bodaboda) 2601 zilizotokea kuanzia Januari hadi
Juni mwaka huu zilisababisha vifo vya madereva 487 wa pikipiki hizo.
Akizungumza
na gazeti hili jana ofisini kwake, Kamishna Msaidi wa Polisi, kikosi
cha usalama barabarani Johansen Kahatano alisema ajali hizo zinazidi
kuongezeka kila mwaka kutokana na sababu mbalimbali.
“Kwa
mwaka 2009 kulitokea ajali 3406 na waliokufa ni 502,mwaka uliofuata
ajali 4363 na vifo 683 na ilipofikia mwaka 2011 zilitpkea ajali zingine
5384 na waliokufa ni 945, taarifa hii inaonyesha kuwa kila mwaka vifo
vinaongezeka”alisema Kahatano.
Alisema
kuongezeka kwa bodaboda na uelewa mdogo wa sheria za usalama barabarani
kwa madereva hao ndiyo sababu kubwa ya ongezeko la ajali hizo.
Alisema
pikipiki zilizo sajiliwa mwaka 2009 kwa ajili ya biashara hiyo ni
87,826 na hadi kufikia mwaka 2011 kulikuwa na pikipiki 1,34,831 na
kwamba wamiliki wake wamekuwa hawana elimu ya kutosha kwa ajili ya
kuwasaidia madereva wao.
Aliongeza
kuwa kutokana na changamoto hiyo wamepata msaada kutoka kwa Taasisi
zisizo za kiserikali kwa mikoa mbalimbali hapa nchini zinazotoa elimu ya
mafunzo ya udereva kwa pikipiki ili kupunguza ongezeko la ajali
“Mafunzo
hayo yalianza Juni mwaka huu,Kwa mkoa wa Tanga kuna taasisi inayoitwa
APEC inatoa mafunzo kwa Bodaboda 2000 hadi sasa na Mkoa wa Mtwara
inaitwa British Gas inatoa mafunzo kwa Bodaboda 600,lengo ni kupunguza
ajali hizi kote nchini”alisema Kahatano.
Hata
hivyo alikiri kuelemewa na utekelezaji wa jukumu la kukamata waendesha
pikipiki wanaovunja sheria barabarani kutokana na wingi wao
ukilinganisha na uchache wa Askari wa usalama barabarani.
Kwa
sasa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Sumatra limeingia makubaliano
na halmashauri zote nchini kuanzia Julai mwaka huu kutoa leseni ya
biashara kwa kila dereva wa bodaboda ili kuwatambua rasmi na kupunguza
matukio ya ukabaji dhidi yao.
Aidha
aliwataka madereva wote na wamiliki wao kutambua sheria za barabarani
na kujali uhai wao pindi wanapokuwa barabarani na kwamba endapo kila
mmoja atafanya hivyo itakuwa ni njia sahihi ya kupunguza au kumalizika
ajali hizo.