OSCAR KUPEWA JEZI YA DROGBA CHELSEA.
KLABU ya Chelsea
imethibitisha kuwa mshambuliaji mpya Oscar anatarajiwa kupewa jezi namba
11 ambayo alikuwa akivaa aliyekuwa mshambuliaji nyota wa klabu hiyo
Didier Drogba ambaye ametimkia katika klabu ya Shanghai Shenhua ya
China. Mchezaji huyo wa kimataifa kutoka Brazil ambaye kwasasa yuko na
timu ya taifa ya nchi hiyo inayoshiriki michuano ya olimpiki atachukua
nafasi ya Drogba ambaye ameondoka klabuni hapo kama mfalme baada ya
kuiwezesha kutwaa taji la Klabu Bingwa ya Ulaya kwa mara ya kwanza msimu
uliopita. Oscar alijiunga na Chelsea inayonolewa na kocha Roberto Di
Matteo kutoka klabu ya Intercional mwezi uliopita kwa ada inayokadiriwa
kufikia paundi milioni 25 na anatarajiwa kupigania nafasi katika kikosi
cha timu hiyo akiwa na wakali wengine kama Eden Hazard, Juan Mata,
Florent Malouda na Daniel Sturridge. Mchezaji huyo mwenye miaka 20
ambaye ana kipaji cha kipekee atafuata nyayo za wakali wengine kama
Damien Duff na Boudewijn Zenden ambao wote walivaa jezi namba 11 kabla
ya kupewa Didier Drogba.