MTANGAZAJI maarufu Bongo anayepiga mzigo katika Runinga ya TBC 1, Amina
Mollel ameangua kilio cha furaha katika sherehe yake ya
kufundwa maarufu zaidi kwa jina la Kitchen Party, ikiwa ni maandalizi ya
ndoa yake.
Tukio hilo limetokea katikati ya wiki iliyopita katika Ukumbi wa Next Door, Tabata jijini Dar es Salaam ambapo ilihudhuriwa na watu wengi maarufu na wasio na majina.
Katika kuonesha tofauti, Amina aliingia ukumbini humo akiongozana na wapambe wake ambapo wote walikuwa wamevaa mavazi ya Kimasai, huku mtangazaji huyo akiwa ameshika fimbo mkononi mwake.
Malkia wa mipasho Afrika Mashariki, Khadija Kopa alitinga ukumbini humo na kuimba nyimbo zake ambazo wanawake wengi wanazipenda, kitendo kilichowainua waalikwa na kuanza kucheza naye.
Baada Khadija kupagawisha, Bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta International’ walivamia jukwaa na kukonga nyoyo za mashabiki kwa sebene safi.
“Ni siku niliyokuwa naisubiri kwa hamu kubwa. Siamini hata
kidogo. Najisikia furaha sana na kila ninayemuona hapa anazidi
kuniongezea furaha ya ajabu moyoni mwangu, ndiyo maana nashindwa
kuyazuia machozi yangu,” alisema Amina.