MARANGU: MVUTA BANGI AUAWA BAADA YA KUMUUA MAMA YAKE


Ingawaje si kweli kuwa walioharibika kwa uraibu wa dawa za kulevya wanaweza kuwekwa kwenye kundi lenye tishio kubwa la kuweza kuutoa uhai wa wanadamu wengine, lakini kila linapotokea tukio moja tayari ni takwimu ambayo inafaaa kurekodiwa, kuchunguwa na kisha kujumuishwa na matukio mengine ili kupata vidokezo muhimu vya jinsi ya kujilinda na kukabiliana na athari hizo. Kila tukio lina mafunzo! Shughuli ipo katika kujifunza kutokana na makosa.

Hivi karibuni, wiki iliyopita, kijana mmoja wa makamo Gift Godlisten Makundi huko nyumbani kwao Komakundi, Marangu-Mamba, Kilimanjaro ameripotiwa kukatiza uhai wa mama yake mzazi, Julitha Godlisten Makundi (57) baada ya kumvamia kwa panga na kisha kumkata kichwa na kukitenganisha na kiwiliwili.

Miili ya marehemu wote ilizikwa na Mchungaji E. J. Mamkwe wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Usharika wa Komakundi, jimbo la Kilimanjaro Mashariki katika Dayosisi ya Kaskazini.

Inaripotiwa na mwanamke aliyefika nyumbani kwa marehemu kushuhudia yaliyotokea, Bi. Angela-Stella W. Temba kuwa kijana aliyesababisha mauaji alikuwa akitumia dawa za kulevya na baadaye kurukwa na akili.



Kwamba, kutokana na matendo yake, mara kadhaa majirani waliwaasa wazazi wake wammfikishe kituo cha polisi, lakini wazazi hawakufanya hivyo. Hatimaye wiki iliopita majira ya saa 9 alasiri siku ya tukio, kijana huyo aliuliza aliko baba yake, ambapo marehemu mama yake alimfahamisha kuwa, ametoka.

Kwamba kijana huyo aliwahi kutamka kuwa atainywa damu ya wazazi wake, lakini maneno hayo yalipuuzwa.

Majirani walipofika baada ya kusikia kelele ya marehemu Julitha na kushuhudia kilichotokea, walimshambulia Gift, wakamponda kichwa na kumwua papo.