MASOUD KIPANYA ARUDI UPYA NA MAISHA PLUS...!

SHINDANO maalum lililotamba miaka nyuma la Maisha Plus, ambalo washiriki wake hukaa kwa miezi miwili kijijini, linatarajiwa kuanza hivi karibuni kwa kushirikiana na shirika la Oxfam Tanzania, kupitia program yake ya ‘Mama shujaa wa chakula’.
Akizungumza kwa jana, Kiongozi Mtendaji wa kampuni ya DMB, Masoud Ali ‘Masoud Kipanya’ alisema kuwa, shindano hilo la aina yake linakuja tena kwa msimu wa tatu, likiwa na utofauti kabisa, huku mambo mbalimbali yakiboreshwa, ikiwemo mshindi kuibuka na kitita cha sh milioni 20.

Kipanya alisema kuwa, kwa kushirikiana na wadhamini wakuu, Oxfam Tanzania, kupitia program yao ya ‘Mama shujaa wa chakula’, ambako watapata fursa ya kuwaweka wanawake kwenye shindano, kwa kukaa ndani ya jumba hilo la Maisha Plus huko kijijini kwa wiki mbili.

“Kwa kushirikiana na Oxfam, shindano hili tumeborsha na litakuwa la aina yake, ambapo washiriki watakaobahatika kushiriki, watafurahia na watajifunza mengi na safari hii Mama shujaa wa chakula nao watabahatika kukaa kwa wiki mbili, kisha watatoka na washiriki wa Maisha Plus kuendelea na kinyang’anyiro cha kuwania kitita hicho cha milioni 20,” alisema Kipanya.

Aidha, aliwataka vijana wa kitanzania, kuchangamkia fursa hiyo, ambako wanatarajia kuanza kufanya usaili mkoani Arusha, Agosti 3 na kisha kuendelea kwenye mikoa mingine 14, ikiwemo ya Bara na viswani Zanzibar.

Pia, alitoa wito kwa wadhamini wengine, kutumia nafasi hii kujitokeza ili kupata kutangaza, kwani shindano hilo licha ya kufanyika misimu miwili ya 2009 na 2010,  huku 2011 likishindwa kufanyika kutokana na kukosa udhamini, limejizolea sifa na kupendwa na watu wa rika mbalimbali.